Wednesday, 15 February 2012

NISHATI ASILIA YA UPEPO
Na Wanderi wa Kamau

Kwa muda mrefu,Wakenya wamekuwa wakiteseka kutokana na ukosefu wa huduma bora za umeme.Hali hii imechangiwa na hali mbaya ya anga ambayo inazidi kubadilika katika miaka ya hivi karibuni hasa kutokana na uharibifu wa mazingira.

Aidha kupungua kwa kiwango cha maji katika miito na mabwawa ambapo mitambo ya kusambazia umeme huwepo vile vile ni kikwazo kikubwa cha huduma duni za usambazaji wa umeme.Lakini swali ambalo Wakenya wanapaswa kujiuliza ni:Je,kuna njia nyengine  wanayoweza kupata nishati mbadala?Kuna njia mwafaka ya nishati asilia?

Mojawapo ya malengo ya milenia ya Umoja wa Mataifa ni kuwa mataifa yote duniani,hasa yaliyo katika bara la Afrika yawe yakijitosheleza kinishati ifikiapo mwaka wa 2015.

Nishati asilia ya upepo ni mojawapo wa njia mwafaka zaidi za kukabiliana na mgogoro wa kinishati unayoikumba dunia nzima,Kenya ikiwepo,hasa wakati binadamu wanapozidi kuongezeka na kuvamia chemichemi na vyanzo vya mito mikuu ambayo huwa aslili ya nishati itumikayo na mataifa mengi.

Aina hii ya nishati ilianza kutumika katika karne nyingi zilizopita.Kwa mujibu wa mtandao wa Wikipidia,mataifa kama vile Denmark na Greece huwa yanatumia nishati hii kwani hakuna mito inayofurika katika mataifa haya yaliyo katika mojawapo ya maeneo baridi sana duniani.

Mtandao huu unazidi kueleza kwamba nishati asilia ya upepo ilikuwa ikitumika na na wafanyabiashara wa asili ya Kiarabu katika karne ya kumi na tisa kusukuma mashua zao kutoka  Bara Arabu(Saudi Arabia na Oman) hadi pwani ya Afrika Mashariki.

Huku kiwango cha misitu ya Kenya kikiwa asilimia 1.7 pekee kufikia mwaka jana,ni muhimu kwa idara husika na Wakenya wenyewe kutafuta njia mbadala za kupata nishati ya matumiziyao ya kila siku.

Kwanza,Kenya lazima ijifunze kutoka kwa nchi ya Rwanda.Kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya nishati duniani katika mwaka wa 2011,Rwanda iliibuka kuwa nchi iliyo na mfumo bora zaidi wa kinishati katika kanda ya Afrika Mashriki katika kudhibiti vituo vyake vya kinishati.

Huku nchi hii ikizidi kuponya makovu ya mauaji ya kimbali ya Aprili 1994,sera zake kuhusu udhibiti wa nishati zimeiwezesha kupiga hatua kubwa hata kiuchumi na kuzipiku baadhi ya nchi ambazo zilikuwa na chumi dhabiti sana katika kanda hii.

Utegaji wa nishati asilia ya upepo si jambo gumu.Huhusisha kuunganisha kifaa kinachofanana na panka ambacho husukumwa na upepo.Kifaa hiki hatimate huunganishwa na mota ambayo hugeuza nguvu hizi hadi kuwa umeme ambao huweza kutumiwa nyumbani kama kupikia na hata viwanda.

Nishati ya upepo  ni asilia.Haina gharama yoyote isipokuwa gharama ya kuziunganisha mashine za kuzigeuza kama vile mota.Manufaa mengine ya aina hii ya nishati ni kuwa inaweza ikatumika kwa matumizi yoyote.Kizingiti chake kimoja tu ni kuwa upatikanaji wake ni wa kimsimu kwa sababu ya mvumo tofauti wa upepo.

Kwa mujibu wa James Njuguna,mkulima katika eneo la Bahati,Nakuru,matumizi ya nishati hii yanaweza yakageuza mgogoro wa ukosefu wa nishati toshelevu hapa nchini."Nimeyatembelea mataifa mbalimbali kwa ufadhili wa shirika la IFAD,na nilivyoona,kupotea au ukosefu wa umeme ni jambo gumu sana katika baadhi ya nchi hizi,Rwanda ikiwemo,"anaeleza.

Mercy Wanjiku,mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Egerton, analaumu mifumo iliyopo ya kinishati hapa Kenya ukiwepo ukuritimba wa taasisi moja katika  kudhibiti ugavi na usambazaji wa  umeme hapa nchini.

No comments:

Post a Comment